BANDARI YA MTWARA YAJIWEKA TAYARI KWA MSIMU WA KOROSHO 2026/2027
Katika kujiandaa na kuanza kwa msimu wa korosho 2026/2027, Bandari ya Mtwara imepokea meli ya kwanza yenye makasha tupu kwa ajili ya kuwezesha usafirishaji wa korosho kwenda katika masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Meli hiyo, MV CONTSHIP ANA II, imewasili katika Bandari ya Mtwara ikiwa na jumla ya makasha tupu 757 (empty containers) ya Kampuni ya MSC, ambayo yataanza kutumika katika shughuli za upakiaji na usafirishaji wa korosho katika msimu huu.
Ujio wa meli hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Bandari ya Mtwara kuhakikisha inakuwa tayari kupokea, kuhifadhi na kusafirisha shehena za korosho kwa ufanisi, wakati mahitaji ya huduma za bandari yanapoongezeka katika kipindi cha msimu.
Maandalizi haya yanaonesha utayari wa Bandari ya Mtwara katika kuhudumia wafanyabiashara na wadau wa sekta ya korosho, huku miundombinu iliyoboreshwa na ufanisi wa huduma ukiendelea kuimarisha nafasi ya bandari hiyo katika kurahisisha usafirishaji wa mazao ya biashara kutoka kusini mwa Tanzania kwenda katika masoko mbalimbali duniani.
Bandari ya Mtwara inaendelea kujiandaa kikamilifu kuhakikisha msimu wa korosho 2026/2027 unahudumiwa kwa ufanisi, kwa wakati na kwa kuzingatia mahitaji ya wadau wa sekta hiyo.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"