Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imesema imeridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Kuhifadhi na Kusambaza Mafuta wa Farm Tank unaotekelezwa 
Kigamboni, pamoja na Mradi wa Kurasini Logistic Centre, unaotekelezwa katika eneo la zamani la EPZA, Kurasini jijini Dar es Salaam. Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo katika miradi hiyo miwili ya kimkakati ya 
Bandari, Septemba 07, 2026, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso (Mb), amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutakuwa na mchango mkubwa katika kukuza biashara, uwekezaji na uchumi wa Taifa. Mhe. Kakoso pia amezipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuendeleza na kuboresha miundombinu ya bandari, akieleza kuwa uwekezaji huo una umuhimu mkubwa katika kuongeza ufanisi wa huduma za bandari na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),

Bw. Plasduce Mbossa, amesema TPA itaendelea kusimamia na kutekeleza miradi ya kimkakati pamoja na maboresho mbalimbali yanayolenga kuongeza ufanisi na ushindani wa Bandari za Tanzania. Amesema utekelezaji wa miradi hiyo, sambamba na maboresho yanayoendelea katika bandari, utasaidia kuongeza uwezo wa kuhudumia na kushughulikia mizigo, kuvutia uwekezaji zaidi na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini. 
Miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya uchukuzi na kuweka mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji. Aidha, miradi hiyo inalenga kuongeza uwezo wa kuhifadhi na kushughulikia mizigo, kuboresha utoaji wa huduma za bandari na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa.