Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mbossa, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake thabiti na uongozi wake mahiri ambao umeifanya sekta ya bandari kuwa kiungo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Bw. Mbossa ametoa pongezi hizo leo tarehe 24 Februari,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma, kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Mamlaka katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.

“ kama mnavyofahamu sekta ya Bandari imekuwa na mabadiliko makubwa tangu Serikali ya awamu ya sita iingie madarakani na sababu kubwa ni uongozi thabiti na maono ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuiimarisha sekta hii na katika hili tunamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais.” Amesema Bw. Mbossa

Amesema kupitia uongozi dhabiti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania inaendelea kujiimarisha kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“ Tunaishukuru Serikali kwani kupitia TPA inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ili kuimarisha miundombinu ya bandari, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma, na kuvutia biashara kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa.” Amesema Bw. Mbossa.

Amesisitiza kuwa TPA itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kwa kuhakikisha uwekezaji unaochochea maendeleo endelevu katika sekta ya bandari unatekelezwa kwa tija na ufanisi wa hali ya juu.

Vilevile, Bw. Mbossa amesisitiza kuwa TPA itaendelea kuhakikisha bandari zinakuwa lango bora la biashara kwa maendeleo ya Taifa.