MRADI WA MATANKI 15 YAMAFUTA WAFIKIA ASILIMIA 52%
Mradi wa kimkakati wa Ujenzi wa Matanki 15 ya Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam wafikia asilimia 52%. Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed amesema kuwa Mradi wa Ujenzi wa matanki 15 ya Mafuta umefikia asilima 52% kukamilika ambapo utapunguza muda wa meli kusubiri, kuondokana na tozo ya ucheleweshaji wa meli (demurrage charges) pamoja na kuongeza ufanisi na mapato. Amesema hayo wakati wa ziara ya timu ya Wahariri na Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea Bandari leo tarehe 3 Septemba 2026, kujionea maendeleo ya miradi ya kimkakati ambayo Serikali kupitia TPA imetekeleza katika kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam katika kuhudumia shehena.
Bw. Abed amesema ujenzi wa mradi huo ulianza rasmi mwaka 2024 ukihusisha ujenzi wa mataki jumla ya 15, ambapo sita (6) kati ya hayo ni kwa ajili ya kupokea shehena ya diseli , matano (5) kupokea shehena ya mafuta ya petroli , matatu (3) kupokea mafuta ya ndege na tanki (1) litakuwa la kazi Maalum (Interface). Matanki yote yatakuwa na uwezo wa kupokea mita za ujazo 378,000 kwa wakati mmoja . Amesema Mradi huo mara utakapokamilika, utapunguza muda wa meli za mafuta kusubiri kutoka siku zaidi ya 30 mpaka kufikia wastanı wa siku 2 kwa kuwa utarahisisha upakuaji kwa haraka pia kuondoa gharama ya tozo inayolipwa na wenye meli ambayo inakadiriwa kuwa jumla ya Dola za Kimarekani 25,000 kwa siku.
“…kupungua kwa gharama za uendeshaji kutapunguza gharama kwa mtumiaji wa mwisho na kama mnavyojua mafuta ni uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa hivyo mradi huu ni muhimu kitaifa na kimataifa kwa kuwa utaongeza uwezo wa Bandari kuhudumia shehena za nchi mbalimbali zinazotuzunguka na kuongeza mapato, ” amesema Bw. Abed. Bw. Abed amewaambia wanahabari hao kuwa ongezeko la shehena limetokana na uwekezaji wa Serikali katika Mradi wa maboresho ya gati, kuongeza kina cha gati na lango la kuingilia meli (DMGP) ambao umewezesha Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa kupokea meli kubwa zenye urefu wa mita 305 na kina (draft) ya mita 15 tofauti ya hapo awali ambapo meli za urefu wa mita 267 na kina cha mita 11 ndio zilizokuwa zinahudumiwa. Kwa upande wa meli Bw. Gallus amesema, meli zinazoingia bandarini sasa zina uwezo wa kubeba jumla ya kontena 8000 TEUs ambapo hapo awali Bandari imehudumia meli zenye uwezo wa kubeba kontena 4000 TEUs. Kwa upande wa meli za kichele, bandari imehudumia meli zenye uwezo wa kubeba tani 70,000 ikiwa ni manufaa kwa wafanyabiashara kwa kuwapunguzia gharama za usafirishaji kwa kuagiza mzigo mkubwa kwa wakati mmoja. Bw. Abed pia ametaja ushirikishwaji wa sekta binafsi kichocheo kikubwa cha ufanisi katika kuhudumiashehena, ambapo Waendeshaji binafsi wamenunua vifaa vipya vya kisasa vyenye uwezo mkubwa ambavyo vimewezesha mzigo kuhudumiwa kwa wakati na kuondolewa kwa wakati ambapo kwa meli za makasha sasa zinakaa wastani wa siku 3 tangu kufika, kuhudumiwa na kutoka tofauti na hapo awali ambapo meli zilikaa kwa siku 30. Wanahabari hao pia wamepata fursa ya kutembelea Gati Na 1-7, Gati maalum ya kuhudumia meli za magari (Gati 0) kujionea shughuli za uhudumiaji wa shehena zinavyofanyika.
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"