MSAJILI WA HAZINA, BW. NEHEMIA MCHECHU AFANYA ZIARA KATIKA BANDARI YA TANGA

Msajili wa Hazina, Bw. Nehemia Mchechu, ameipongeza Menejimenti na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kazi nzuri ya kusimamia rasilimali za Serikali kwa ufanisi na weledi.
Bw. Mchechu ametoa pongezi hizo alipofanya ziara ya kikazi katika Bandari ya Tanga, ambapo alikagua shughuli za kiutendaji na kujionea maendeleo ya miradi mbalimbali ya maboresho ya bandari hiyo, inayotekelezwa na Serikali kupitia TPA.
“Bandari ni kiwanda cha pesa cha Serikali. Sehemu kubwa ya mapato ya TRA yanatokana na shughuli za bandari. Ofisi yangu inaiangalia TPA kwa jicho la kipekee kwa sababu mchango wake katika mapato ya taifa ni mkubwa sana,” alisema Bw. Mchechu.
Ameeleza kuwa ofisi yake inafarijika na huduma zinazotolewa katika Bandari ya Tanga, akisisitiza kuwa mafanikio yanayoonekana ni matokeo ya mshikamano na bidii za menejimenti pamoja na watumishi wa TPA.
Aidha, aliwataka wafanyakazi wa TPA kuendelea kuthamini kazi zao na kujivunia utumishi wao ndani ya mamlaka hiyo, akieleza kuwa bandari ni “mboni ya jicho la Serikali.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa, amesema mamlaka hiyo itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwa niaba ya Serikali ili kuhakikisha Bandari ya Tanga inajengeka kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Alibainisha kuwa Serikali imewekeza Shilingi bilioni 429.1 katika maboresho ya awali ya bandari hiyo, na tayari uwekezaji huo umeanza kuleta tija kwani mapato yanayokusanywa na TPA kwa kushirikiana na TRA katika kipindi cha miaka miwili yamerudisha gharama hizo.