Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Abdallah Mitawi, tarehe 17 Septemba 2026 amefanya ziara katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ikiwa na lengo la kufahamu kwa kina shughuli zinazotekelezwa na Mamlaka hiyo pamoja na mchango wa bandari katika kukuza biashara, usafirishaji na uchumi wa Taifa. Katika ziara hiyo, Bw. Mitawi amepokelewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mha. Dkt. Baraka Mdima, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA. Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Mitawi ameipongeza Menejimenti ya TPA kwa mafanikio yaliyopatikana katika kuhudumia shehena na kuongeza mapato kupitia bandari 
zinazosimamiwa na Mamlaka hiyo. Amesema mafanikio hayo yanadhihirisha umuhimu wa kuendelea kuboresha ufanisi wa huduma za bandari, kuimarisha matumizi ya teknolojia na ubunifu, pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wadau wa sekta ya usafirishaji.

Amesisitiza kuwa bandari ni kiungo muhimu katika mnyororo wa biashara na usafirishaji, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuimarisha miundombinu, mifumo ya uendeshaji na huduma za bandari ili kuongeza ufanisi na ushindani wa bandari za Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Aidha, Bw. Mitawi amesisitiza umuhimu wa TPA kuwa na mipango na mikakati inayokwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ili kuhakikisha sekta ya bandari inatoa mchango unaostahili katika kufanikisha malengo ya Taifa. Amesema utekelezaji wa Dira hiyo kupitia bandari za TPA unapaswa kuchangia katika kuongeza mapato ya Taifa, kuzalisha ajira na kuwezesha Sekta Binafsi kutimiza lengo la kuchangia asilimia 70 ya shughuli za kiuchumi nchini. 

Kwa upande wake, Mha. Dkt. Baraka Mdima amemshukuru Naibu Katibu Mkuu kwa kutembelea TPA na kueleza kuwa Mamlaka itaendelea kutekeleza kwa ufanisi maelekezo na mipango ya Serikali katika kuboresha huduma za bandari na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa. Dkt. Mdima amesema TPA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji na biashara, wakiwemo wadau kutoka Sekta Binafsi, katikakuongeza ufanisi na tija katika sekta ya bandari, kuboresha huduma za kuhudumia na kushughulikia mizigo, pamoja na kuimarisha ushindani wa bandari za Tanzania. Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Uchukuzi na TPA za kuimarisha ushirikiano na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mikakati ya Serikali katika kuendeleza sekta ya usafirishaji, kukuza biashara na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.