Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mbossa amesema kuwa wamejipanga kufanya upanuzi wa Bandari za Mamlaka ili kuendelea kutoa huduma shindani katika soko la Afrika na Kimataifa.

Akizungumza hivi karibuni, Mbossa amesema kuwa TPA imejiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kiushindani kutokana na uwekezaji wake unaoendelea katika bandari mbalimbali hapa nchini.

Moja ya mikakati hiyo ni pamoja na mpango wa kupanua na kujenga gati 10 katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza ufanisi na tija katika bandari hiyo.

“Katika kuhakikisha wateja wetu wanaendelea kupata huduma bora na stahiki sisi kama mamlaka tumekuja na mpango wa kuongeza gati 10 katika bandari ya Dar es salaam,”

“Hii inaenda kupanua soko la biashara kwa watumiaji wa bandari yetu kwani ufanisi utakuwa ni mkubwa na utakidhi mahitaji ya wateja wetu”, amesema.

Aliongeza kusema TPA imeendelea kuboresha miundombinu ya bandari zake ambazo ni pamoja na bandari ya Bagamoyo, Bandari ya Tanga, Mtwara, Mbamba Bay na bandari zingine ambazo ziko chini ya mamlaka hiyo.

Amesema hayo yote yanafanyika ili kuhakikisha kuwa TPA inachochea uchumi wa Taifa kupitia Bandari zake kwa kushirikiana na wawekezaji waliopo.

“TPA tumejipanga kuufungua uchumi wa Taifa kwa kutumia bandari zetu na ndio maana tumeendelea kuboresha maeneo mengi ya bandari zetu ili ziweze kutoa huduma kwa wateja wetu wa ndani na nje ya nchi.”

“Kwa kupitia uwekezaji ambao tumeufanya katika bandari zetu, matunda yake tumeanza kuyaona ambapo hadi sasa kumekuwa na utofauti mkubwa katika huduma za bandari ukilinganisha na miaka kadhaa ya nyuma”

“Hii inatokana na juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuleta mageuzi makubwa ya kiutendaji katika bandari zetu ili kuchochea biashara zaidi na kukuza uchumi wa nchi yetun”amesema Bw. Mbossa.