Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeungana na Watanzania na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kusisitiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira ili kuhakikisha maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani hufanyika kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 5 Juni kwa lengo la kuhamasisha jamii duniani kote kuchukua hatua madhubuti za kulinda na kuhifadhi mazingira. 
Kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yanaongozwa na kauli mbiu ya kitaifa isemayo, “DIRA 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”Taarifa ya TPA imeeleza kuwa mazingira ni nguzo muhimu ya maisha na maendeleo ya binadamu kwa kuwa yanatoa huduma muhimu kama hewa safi, maji, chakula, malighafi za viwandani na makazi. Aidha, maendeleo ya kijamii na kiuchumi hayawezi kufikiwa bila kuwepo kwa mazingira salama na yanayohifadhiwa ipasavyo.Katika kuunga mkono juhudi za Serikali za uhifadhi wa mazingira, TPA imeendelea kuhakikisha shughuli zote za uendeshaji wa bandari na utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinafanyika kwa kuzingatia misingi ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira. 

Mamlaka hiyo pia inaendelea kutekeleza Sera yake ya ‘Green Port Policy’, inayolenga kuendeleza bandari rafiki kwa mazingira na zinazochangia maendeleo endelevu ya taifa.TPA imebainisha katika taarifa yake kuwa Dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimazingira zikiwemo ukataji miti ovyo, uchafuzi wa mazingira, matumizi holela ya plastiki, mabadiliko ya tabianchi pamoja na uharibifu wa vyanzo vya maji. Changamoto hizo zinaendelea kuathiri afya za wananchi, uzalishaji wa kilimo, bioanuwai na ustawi wa jamii kwa ujumla.Mamlaka hiyo imewataka wananchi na wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuhifadhi mazingira kwa kupanda na kutunza miti, kutumia kwa uangalifu rasilimali za asili kama maji, umeme na mafuta, kulinda vyanzo vya maji, kupunguza matumizi ya plastiki zisizorejelewa na kuhakikisha taka zinahifadhiwa na kutupwa katika maeneo sahihi. 

“Hatua ndogo tunazochukua kila siku zina mchango mkubwa katika kulinda mazingira yetu. Ushirikiano wa wananchi, taasisi na wadau mbalimbali ni muhimu katika kujenga mazingira safi, salama na endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” imeeleza TPA .TPA imewataka wananchi kutumia maadhimisho hayo kama fursa ya kutafakari mchango wao binafsi katika uhifadhi wa mazingira na kuwa mabalozi wa mazingira katika familia, maeneo ya kazi na jamii wanamoishi.
Kwa pamoja, jamii inaweza kuchangia kujenga Tanzania yenye mazingira bora kwa maendeleo endelevu, sambamba na kufanikisha azma ya taifa ya kuwa na uchumi wa 
kijani unaolinda rasilimali za asili kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.