Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeibuka Mshindi wa Tatu katika Kundi la Taasisi Umma zinazozingatia na kufuata Miongozo na Kanuni za Mamlaka ya Serikali Mtandao katika uendeshaji na usimamizi wa mifumo ya TEHAMA katika shughuli zake.

TPA imepata jumla ya asilimia 91.11 katika Tathmini ya uzingatiaji wa Kanuni na Miongozo inayotolewa na e-GA katika uendeshaji Serikali Mtandao.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Mhe. George Boniface Simbachawene amefunga Kongamano la 5 la Mwaka la Serikali Mtandao, tarehe 13 Februari, 2025 jijini Arusha na kuwaelekeza Viongozi na watumishi wa Umma kuzingatia na kutekeleza maazimio 6 ya Kikao hicho ipasavyo.

Mhe. Simbachawene amehimiza umuhimu wa kutekeleza maazimio hayo ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuboresha huduma za Serikali kwa wananchi wake kwa mifumo ya kidigitali.

Kongamano hilo lililokuwa na Kauli Mbiu “ Huduma za Serikali Mtandao na ubunifu wa Utoaji Huduma za Mifumo ya TEHAMA kwa wananchi kwa ufanisi” limejadili jitihada za e-GA katika kujenga Serikali mtandao.

Masuala mengine yaliyojiri katika kikao hicho ni kubainisha fursa na changamoto za utekelezaji Serikali Mtandao pamoja na mbinu bora za kufanikisha na kuendesha Serikali Mtandao. Kongamano la 5 la Mwaka la Serikali Mtandao limehudhuriwa na washiriki zaidi ya 1,000 kutoka Seriikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na Mamlaka za umma, Sekta Binafsi na Wataalamu kutoka nje ya Nchi.