Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Abdallah Mussa Mwaipaya, ameipongeza Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) kwa kuimarisha miundombinu ya Bandari ya Mtwara, inayochangia kuongeza uwezo wa Bandari hiyo katika uhudumiaji wa shehena ikiwemo za mazao ya biashara.
Mhe. Mwaipaya amesema hayo alipotembelea banda la TPA katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini ambayo yanafanyika katika Viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi.
Aidha, Mhe. Mwaipaya amesema uwekezaji wa miundombinu ya Bandari na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kuhudumia shehena ni vitu ambavyo Wilaya ya Mtwara inajivunia kwa kuwa umechangia kuhudumia kwa ufanisi zao la korosho.
TPA inatumia jukwaa la Maonesho ya Nanenane ambayo Kitaifa yanafanyika Jijini Dodoma, katika kuonesha uhusiano uliopo baina ya shughuli za kibandari na Sekta ya Kilimo Nchini.