Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame M. Mbarawa ameiagiza TPA ifikapo Novemba 2026 eneo la wazi la EPZA kurasini kuanza kazi rasmi ya kuhudumia shehena inayoingia katika Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza ufanisi.
Mhe. Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo tarehe 21 Agosti 2026 mara baada ya kufanya ziara katika eneo hilo kujionea maendeleo ya mradi huo uliofikia asilimia 98.
Amesema kuwa eneo hilo litatumika kama sehemu ya eneo la Bandari na Taasisi zote muhimu zitakuwepo hapo na Wananchi kuchukua mizigo katika eneo hilo ambalo litaongeza ufanisi wa bandari katika kuhudumia shehena.
Waziri Mbarawa pia amesema eneo hilo litakapokamilika linatazamiwa kuifadhi mizigo inayoshushwa katika Bandari ya Dar es Salaam na kuipa nafasi kuhudumia shehena nyingine inyoingia bandarini hapo.
“Mradi huu utapunguza mzigo unaoshushwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa mzigo utakapofika utapelekewa moja kwa moja katika eneo hilo ambalo kwa sasa katika awamu ya kwanza ya ujenzi linauwezo wa kuhudumia makasha 150,000 TEUS na awamu ya pili litakuwa na uwezo wa kuhudumia makasha laki 7 (700,000) TEUS” Amesema Waziri Mbarawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed amesema kuwa ndani ya Mwaka mmoja 2024/2025 kumekuwa na ongezeko kubwa la shehena la tani Milioni sita(6) hivyo Serikali ikachukua hatua ya kimkalati ya kutumia eneo hilo kuwa sehemu ya Bandari ili kuhudumia shehena kubwa zaidi.
Amesema eneo hilo litahifadhi Malori na shehena kabla haijaondoka katika Bandari ya Dar es Salaam.