WAZIRI MKUU AMEKAGUA MABASI 99 YA MWENDO KASI KATIKA BANDARI YA DAR ES SALAAM

Waziri Mkuu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, tarehe 13 Agosti 2025 amekagua mabasi 99 ya Kampuni ya Mofat katika Bandari ya Dar es Salaam na kuwaagiza kuanza kutoa huduma ya usafiri ndani ya siku 7.
Mabasi hayo yatatoa huduma katika njia ya kuanzia katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwenda Mbagala.
Mhe. Majaliwa ameishukuru Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kuwezesha magari hayo kushushwa Bandarini kwa haraka na kuhifadhiwa kwa muda katika yadi ya magari (RoRo).
Kwa kuwa taratibu zote za kibandari zimekamilika, Mhe. Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mofat Bw. Abdallah Kassim kuyaondoa mabasi hayo kwa wakati ili kutoa nafasi ya kuhudumia mizigo ya Wateja wengine.
Mhe. Waziri Mkuu aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu) Mhe. William Lukuvi , Naibu Waziri wa Tamisemi Mhe. Zainab Katimba, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi, Mkurugenzi Mkuu wa (DART) Dkt. Athuman Kihamia, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolona na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Mara baada ya kufika Bandarini, Mhe. Waziri Mkuu amepokelewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mha. Dkt. Baraka Mdima kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu TPA Bw. Plasduce Mbossa, pamoja na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed Gallus na watendaji wengine wa Mamlaka.