Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kuboresha huduma za bandari, akieleza kuwa uwekezaji unaoendelea kufanywa pamoja na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi umeanza kuzaa matunda kupitia ongezeko la mapato, shehena zinazohudumiwa na ufanisi wa utoaji wa huduma.Mhe. Balozi Omar ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la TPA katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alipata fursa ya kujionea maboresho mbalimbali yaliyotekelezwa na Mamlaka katika kuendeleza sekta ya bandari nchini.“Nimefurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na TPA. Ushirikiano wake na wawekezaji unaoendesha shughuli za bandari umeleta matokeo chanya yanayoonekana kupitia kuongezeka kwa mapato, shehena zinazohudumiwa na ufanisi wa huduma. Haya ni mafanikio yanayochangia ukuaji wa uchumi wa Taifa,” alisema Waziri wa Fedha.
Aidha, Waziri huyo aliishauri TPA kuendelea kuwekeza kikamilifu katika matumizi ya Bandari Kavu ya Kwala ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi na kusambaza shehena, hatua ambayo itasaidia kupunguza msongamano wa malori katika Bandari ya Dar es Salaam na kwenye mtandao wa barabara za Jiji la Dar es Salaam.Vilevile, aliwataka wawekezaji wanaoshiriki katika shughuli za bandari kuweka mkakati wa kujenga barabara maalum za kuunganisha maeneo ya shughuli za kibandari (access roads), hatua itakayorahisisha uhamishaji wa shehena kutoka bandarini kwenda Bandari Kavu ya Kwala na maeneo mengine ya kimkakati, sambamba na kuongeza ufanisi katika mnyororo wa usafirishaji.TPA inaendelea kutumia Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam kama jukwaa la kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma za bandari, maboresho ya miundombinu, matumizi ya teknolojia za kisasa na fursa mbalimbali za uwekezaji zinazoiwezesha Tanzania kuendelea kuwa lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.