Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ametembelea Bandari ya Tanga, Julai 13, 2026, na kujionea mafanikio makubwa yaliyopatikana baada ya maboresho ya bandari hiyo yaliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, Mhe. Balozi Omar, alipokea taarifa ya utendaji kutoka kwa Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Salehe Mbega, iliyoonesha ongezeko kubwa la meli, shehena, mapato na ajira kufuatia uwekezaji wa Serikali. Mhe. Balozi Omar, ameipongeza Menejimenti ya TPA kwa usimamizi mzuri wa maboresho hayo na kuagiza utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya mradi wa ujenzi wa magati matatu mapya uanze mara moja ili kuongeza uwezo wa kuhudumia meli na kukidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka.