Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeandaa na kuratibu zoezi la pamoja la ulinzi wa bandari kwa njia ya majadiliano (Joint Port Security TableTop Exercise) litakalofanyika tarehe 08 Oktoba, 2026 katika bandari ya Dar es Salaam.

Zoezi hili litahusisha maeneo manne (4) ya kiutekelezaji ambayo ni DP World Terminal, TEAGTL Terminal, Kurasini Oil Jetty (KOJ) na Single Buoy Mooring (SBM).

Zoezi hili ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya  Sheria ya Kimataifa ya Ulinzi na Usalama wa Meli na Bandari (International Ship and Port Facility Security (ISPS) Code) kwa lengo la kupima na kuimarisha utayari, uwezo na ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kukabiliana na tukio kubwa la kiusalama linaloweza kutokea katika eneo la bandari.

Zoezi hili linalenga kuhakikisha Bandari ya Dar es Salaam inaendelea kuwa salama, imara na yenye uwezo wa kuhimili na kukabiliana kwa ufanisi na matukio ya kiusalama, sambamba na kuendelea kuzingatia matakwa ya kitaifa na viwango vya kimataifa vya ulinzi na usalama wa meli na Bandari.

Manufaa ya zoezi hilo ni pamoja na, kuimarisha uratibu miongoni mwa taasisi na wadau katika kubaini, kuzuia na kukabiliana na vitendo vya uhalifu bandarini na kupima ufanisi wa mifumo ya taarifa na mawasiliano kati ya wadau mbalimbali wakati wa tukio la kiusalama.

Malengo mengine ya zoezi hili ni kutathmini namna sahihi na kwa wakati ya kukabiliana na tukio la uhalifu, kwa kuzingatia majukumu na mamlaka ya kila Taasisi sambamba na

kubaini mapungufu, changamoto na maeneo yanayohitaji maboresho katika mipango na taratibu za ulinzi wa bandari ili kuongeza ufanisi wa kukabiliana na matukio ya kiusalama.

Wadau wanaoshiriki zoezi hilo ni vyombo  vya ulinzi na usalama, ikijumuisha Jeshi la Polisi Tanzania, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Usalama wa Taifa na Idara ya Ulinzi ya TPA.

Wadau wengine ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), mawakala wa meli, mawakala wa forodha, DP World, TEAGTL, pamoja na watumiaji wengine wa Bandari.