Bandari ya Mtwara imeendelea kuhudumia meli za aina mbalimbali ambapo tarehe 18.01.2026 imepokea meli ya mizigo ya MV ANTHIA iliyobeba shehena ya magari pamoja na mitambo ya ujenzi wa miradi mbalimbali kutoka Nchini China.
Meli hiyo imeshusha jumla ya mizigo 323 yenye uzito wa tani 2,448.91. Mizigo hiyo imewasili kwa ajili ya kusafirishwa kwenda kwa wateja mbalimbali waliopo Nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia, Malawi na Burundi.
Akizungumzia kuhusu ujio wa meli hiyo, Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara Kapteni Paul Mchwampaka amesema kuwa, hatua hiyo inaendelea kufungua milango ya kibiashara kwa Bandari ya Mtwara pamoja na kuchochea nafasi ya Bandari katika kuvutia Nchi jirani kupitishia shehena zake.
Kwa upande wa Wakala wa Kampuni ya Seafront Shipping Service Limited iliyoleta meli hiyo Bw. Erick Anthony ameonesha kuridhishwa na huduma zinazotolewa katika Bandari ya Mtwara. Wakala huyo amesisitiza dhamira ya kuendelea kuleta meli nyingi zaidi za aina hiyo katika Bandari ya Mtwara akieleza kuvutiwa na ufanisi mkubwa, weledi wa watendaji na ubora wa vitendea kazi vilivyopo Bandarini hapo.


Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Salehe Mbega ametoa rai kwa wadau wa usafirishaji wa bandari hiyo kukitumia Chama cha Madereva wa Masafa Marefu (CHAMATTA) Mkoa wa Tanga ambacho kwa sasa kinatambulika kihalali baada ya kupata vibali vyote kutoka mamlaka husika.
Bw. Mbega alitoa rai hiyo kwenye uzinduzi wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la “Bandari House”
Akiongea katika uzinduzi huo Bw. Mbega alisema kuwa, uwepo wa chama hicho katika Mkoa wa Tanga utasaidia kuibua fursa za ajira hususani madereva ambao ndio mhimili wa usafirishaji wa mizigo katika Bandari ya Tanga.
“Bandari ya Tanga imekuwa na ongezeko kubwa la shehena ya magari yanayoshuka kwa wastani wa magari 1500 kwa mwezi ambapo asilimia 70 ni magari yanayoenda nchi jirani “Transit” hivyo nawaasa madereva kutumia fursa ya ajira kupitia CHAMATTA “. Aliongeza Bw. Mbega
Katika hatua nyingine Bw. Mbega alikitaka chama hicho kusimamia maadili kwa madereva ili kujenga uaminifu na kuweka imani kwa wateja wanaopitisha mizigo Bandari ya Tanga.
Awali akitoa utambulisho kwa viongozi wa chama hicho, Mwenyekiti wa CHAMATTA Mkoa wa Tanga Bw. Adamu Mwenda alisema kuwa, kuanzishwa kwa chama hicho Mkoa wa Tanga ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Aidha Bw. Mwenda aliipongeza Bandari ya Tanga kwa ushirikiano na kuthamini mchango wa madereva wa masafa marefu “Transit” Mkoa wa Tanga hivyo alitoa wito kwa wadau wa usafirishaji kukitumia chama hicho.


Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 10.08 katika miradi 22 ya ujenzi, upanuzi na maboresho ya bandari kote nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha miundombinu ya usafiri wa majini na kukuza uchumi wa taifa.
Prof. Mbarawa ameyasema hayo tarehe 17 Januari, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bandari mpya ya Mbamba Bay, iliyopo Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza na viongozi wa Serikali, wataalamu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na wananchi wa eneo hilo, Prof. Mbarawa amesema uwekezaji huo mkubwa unaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
Ameeleza kuwa ujenzi wa Bandari mpya ya Mbamba Bay kwa shilingi Bilioni 81 ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa chini ya Wizara ya Uchukuzi, hususani katika Maziwa Makuu, kwa lengo la kuimarisha biashara ya kikanda na usafiri wa majini katika Ziwa Nyasa.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mha. Dkt. Baraka Mdima, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, amesema mradi wa Bandari ya Mbamba Bay umefikia Asilimia 47 ya utekelezaji wake, na unaendelea kutekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu, usalama na utunzaji wa mazingira.
Dkt. Mdima aliongeza kuwa kukamilika kwa bandari hiyo kutachochea biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Malawi na Msumbiji, sambamba na kuongeza ajira, uwekezaji na fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Naye Mhandisi Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay kutoka TPA, Bw. John Paul, alitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu maendeleo ya mradi, akibainisha kuwa kazi zinaendelea vizuri na kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kupeleka miradi mikubwa ya maendeleo mkoani humo, akisema bandari hiyo itakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Nyasa na maeneo ya jirani.
Mradi wa ujenzi wa Bandari mpya ya Mbamba Bay unatarajiwa kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Nyasa, kuchochea biashara kati ya Tanzania na Nchi jirani zikiwemo za Malawi na Msumbiji na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya kikanda.



Serikali ya Jamhuri ya Zambia imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina yake na Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati wa Zambia Prof.Ephraim Munshifwa alipofanya ziara Bandari ya Dar es Salaam katika eneo linalohudumia meli za mafuta Kurasini Oil Jet (KOJ) na kwenye boya linaloelea baharini (Single Mooring Point - SPM) Januari 16,2026.
Katika salamu zake za ukaribisho alizozitoa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce M Mbossa, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed ameishukuru nchi ya Zambia kwa kuendelea kutumia Bandari ya Dar es Salaam na kuainisha kuwa ufanisi wa Bandari umeongezeka kutokana na uwekezaji uliofanyika kwenye miundombinu sambamba na ushirikishwaji wa waendeshaji binafsi katika Bandari.
Aidha, Bw. Gallus ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia tani milioni 27.7 na mwaka 2025/2026 inatarajia kuhudumia zaidi ya tani milioni 32. Ongezeko hili linatokana na ufanisi pamoja na imani ya wateja kwa huduma za Bandari ya Dar es Salaam.
Tanzania na Zambia zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu wa kibiashara kupitia mradi wa bomba la mafuta la Tanzania - Zambia (TAZAMA) lenye urefu wa kilometa 1710 linaloanzia Dar es Salaam mpaka Ndola Zambia.


Bandari ya Kilwa imeendelea kupokea na kuhudumia meli za Kitalii ambapo tarehe 15 Januari 2026 meli iitwayo MV ISLAND SKY imewasili ikiwa na jumla ya watalii 89 pamoja na wafanyakazi wa meli 79.
Watalii hao wanatoka nchi za Uingereza, Uholanzi, Ireland, Ujerumani, Finland na Australia ambao wamewasili katika Mji wa Kilwa kwa lengo la kutembelea vivutio mbalimbali vya asili vyenye kubeba historia kubwa ya Afrika Mashariki ambavyo vimekuwa vikitangazwa kwa nia ya kukuza Utalii katika Ukanda wa Kusini na Tanzania kwa ujumla.
Vilevile, Watalii hao wamepata fursa ya kujionea mradi mkubwa unaoendelea wa ujenzi wa Bandari ya Kisasa ya Uvuvi katika Bandari ya Kilwa. Wageni hao wamepongeza hatua hiyo na kusisitiza kuwa, kuongezeka kwa vivutio vya Utalii pamoja na miundombinu bora ya Bandari vitachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la idadi ya Watalii wanaotembelea eneo hilo siku kwa zijazo.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mkuu wa Idara ya Ubaharia Kapteni Paul Mchwampaka amesema, Bandari itaendelea kuhudumia meli za Utalii kwa ufanisi mkubwa ili kuendelea kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan za kukuza Sekta ya Utalii ambayo ni nguzo kubwa katika kuitangaza nchi na kuongeza pato la Taifa.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"