Wafanyakazi Bandari ya Dar es Salaam wamepongezwa kwa kuhudumia shehena tani Mil. 13.99 kwa kipindi cha miezi mitano, kuanzia Julai mpaka Novemba 2025 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed wakati akifungua Kikao cha 75 cha Kamati ya Utendaji Bandari ya Dar es Salaam, kinachofanyika mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Amesema kuwa kipindi kama hiki cha miezi mitano 2024/2025, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia shehena tani mil. 10.48 ikiwa ni tofauti ya tani 3.51 sawa na 33.5%.
Ameongeza kwa kusema kuwa, kwa mwenendo huo inatarajiwa mpaka kufika mwisho wa mwaka 2025/2026 Bandari ya Dar es Salaam itahudumia tani mil.32.
Aidha Bw. Galus amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi kati ya Menejimenti ya Bandari ya Dar es Salaam na Wafanyakazi kwa kushirikiana na Wadau na wawekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam yanayopelekea kufikia malengo ambayo Bandari ya Dar es Salaam imewekewa na Serikali.
Kikao cha Kamati ya Utendaji kitakaa kwa siku mbili, kikifuatiwa na Kikao cha 75 cha Baraza la Wafanyakazi kituo cha Bandari ya Dar es Salaam kitakachofanyika tarehe 16 Januari 2026.


Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Watumishi wote wa Mamlaka ya Usimamamizi wa Bandari Tanzania (TPA), tunawatakia Wazanzibari na Watanzania wote, heri ya kumbukizi ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Serikali imeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kuendelea kuboresha uendeshaji wa bandari nchini, hatua iliyoongeza ufanisi, uwajibikaji na ubora wa huduma, sambamba na kuimarisha mchango wa bandari katika kukuza uchumi wa Taifa.
Akizungumza mkoani Pwani baada ya kutembelea Bandari ya Nyamisati, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe.David Kihenzile, amesema maboresho yanayotekelezwa na TPA yameifanya sekta ya bandari kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi kwa kuongeza kasi ya kuhudumia mizigo, kupunguza muda wa meli kukaa bandarini na kuboresha mazingira ya biashara.
Alisema hatua hizo zimeendelea kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango muhimu la biashara na usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mhe. Kihenzile ameitaka TPA kuhakikisha miradi ya ujenzi wa bandari za Bagamoyo, Kisiju na Nyamisati inawanufaisha wananchi moja kwa moja kupitia utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), ikiwemo huduma za kijamii na uboreshaji wa miundombinu katika maeneo yanayozunguka bandari.
Kuhusu usafiri wa uhakika katika bahari kuu, Naibu Waziri Kihenzile amesema Serikali kupitia Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) inaendelea na tafiti za kitaalamu ili kubaini mahitaji halisi, kama sehemu ya maandalizi ya kuchukua hatua za kuimarisha usafiri majini nchini.
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus, amesema maboresho yanayotarajiwa kufanyika ni pamoja na uboreshaji wa jengo la abiria ili liweze kuhudumia abiria 300 kwa wakati mmoja, pamoja na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mingine ya bandari.


Wadau wa Bandari ya Tanga wameipongeza Menejimenti ya Bandari hiyo, kwa juhudi kubwa walizofanya kuhakikisha kunakuwa na meli za moja kwa moja za shehena ya Makasha.
Wadau hao wametoa pongezi hizo wakati wa Kikao cha Kamati ya Maboresho ya Bandari ya Tanga (Port Improvement Committee - PIC) kilichojumuisha wadau mbalimbali kutoka Sekta binafsi na Taasisi za Serikali.
Wadau hao wamesema uwepo wa meli ya Makasha ya moja kwa moja kutoka nchini Irani mpaka katika Bandari ya Tanga itaondoa changamoto ya muda mrefu ya Bandari ya Tanga kupokea meli ndogo ndogo ‘Feeder ‘kutoka Bandari za nchi jirani ambazo zimekuwa zikisababisha Shehena nyingine kukosa nafasi katika meli hizo.
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Salehe Mbega amewataka wadau hao kuwasilisha changamoto zao kwa wakati pindi zinapojitokeza ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora wakati wote.



Kwa mara ya kwanza katika historia, Bandari ya Mtwara inatarajiwa kuanza kupokea mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa uchimbaji wa gesi asilia katika eneo la Nanguruwe, Mkoa wa Mtwara.
Hatua hiyo imebainika baada ya ugeni wa wafanyabiashara na viongozi wa Kampuni ya ARA Petroleum Tanzania kufanya ziara maalum katika Bandari ya Mtwara kwa lengo la kujiridhisha na uwezo wa bandari hiyo kuhudumia shehena kubwa za mitambo ya mradi huo kuanzia mwezi Agosti, 2026.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Meneja wa ARA Petroleum Tanzania, Bw. Hilal Al Hinai, amesema lengo la ziara hiyo lilikuwa kutathmini miundombinu, vitendea kazi pamoja na ufanisi wa bandari katika kushughulikia mizigo mizito na mikubwa.
Amefafanua kuwa kuanzia mwezi Agosti, 2026, kampuni hiyo inatarajia kuanza kupokea meli zitakazobeba vifaa vya mradi huo, ambapo kila meli itakuwa na zaidi ya tani 1,000 za mitambo na vifaa mbalimbali vitakavyotumika katika uchimbaji wa gesi eneo la Nanguruwe.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mkuu wa Idara ya Masoko, Bw. Faraji Mbulalina, amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wengi zaidi kutumia bandari hiyo, akieleza kuwa ina uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena mbalimbali kwa ufanisi.
Bw. Mbulalina amesema Bandari ya Mtwara imeendelea kuboreshwa na kwa sasa ina unafuu wa tozo za kibandari, miundombinu wezeshi, vitendea kazi vya kisasa pamoja na rasilimali watu wenye ujuzi na weredi wa hali ya juu, hivyo kuwa chaguo sahihi kwa miradi mikubwa ya kimkakati.
ARA Petroleum Tanzania ni kampuni ya uchimbaji na uzalishaji wa mafuta na gesi, inayojihusisha na maendeleo ya rasilimali za gesi asilia katika eneo la Ntorya – Mtwara Kusini. Kampuni hiyo ni tawi la ARA Petroleum yenye makao yake nchini Oman, iliyoanzishwa kusimamia na kuendeleza mradi wa gesi uliogunduliwa chini ya Ruvuma Production Sharing Agreement (PSA).
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"