Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akiwa katika ziara yake inayoendelea Mkoani Lindi, tarehe 21 Disemba 2025 ametembelea Bandari ya Lindi na kujionea shughuli mbalimbali za utekelezaji katika Bandari hiyo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri Mkuu alipokea taarifa fupi ya utendaji kazi wa Bandari ya Lindi kutoka kwa Meneja wa Bandari ya Mtwara Bw. Ferdinand Nyathi ambaye alieleza kuhusu hali ya uendeshaji wa Bandari ya Lindi, mafanikio yaliyopo pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili Bandari hiyo kwa sasa.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack ameeleza kuwa, Bandari ya Lindi inakabiliwa na changamoto ya kujaa mchanga katika eneo la gati hali inayosababisha kupungua kwa kina cha Bandari na hivyo kuathiri uwezo wa kuhudumia meli hususan meli za mizigo mchanganyiko ambazo zinahitaji uwepo wa kina kirefu.
Baada ya kupata maelezo yote hayo, Mhe. Waziri Mkuu alitoa maagizo kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuharakisha mchakato wa kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Bandari mbadala.


Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa Usanifu na Ujenzi wa Bandari Mpya ya Kisiwa Mgao, mkoani Mtwara, ambao umefikia asilimia 25 ya utekelezaji wake.
Akizungumza baada ya ziara yake ya kutembelea na kukagua mradi huo,tarehe 20 Disemba,2025, Waziri Prof. Mbarawa ameeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji pamoja na ubora wa kazi zinazoendelea kufanyika katika eneo la mradi.
Waziri Prof. Mbarawa amesema Bandari mpya ya Kisiwa Mgao ni mradi wa kimkakati unaolenga kuimarisha sekta ya uchukuzi wa majini na kukuza uchumi wa Taifa, hususan kwa ukanda wa Kusini, hivyo ni wajibu wa TPA na wadau wote kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kuzingatia ubora, uwazi na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.
Aidha, Waziri Mbarawa alibainisha kuwa kukamilika kwa Bandari ya Kisiwa Mgao kutaongeza uwezo wa nchi katika kuhudumia shehena ya mzigo mchafu, kupunguza msongamano wa shughuli za bandari ya Mtwara, na kuimarisha biashara pamoja na usafirishaji wa bidhaa katika ukanda wa Kusini na nchi jirani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa, amesema mradi huo utakuwa chachu kubwa ya maendeleo ya kiuchumi kwa mkoa wa Mtwara na maeneo ya jirani kwa kuongeza fursa za ajira, kuchochea shughuli za kibiashara, na kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa bidhaa za kimkakati, hususan makaa ya mawe, saruji na mbolea.
Bw. Mbossa aliongeza kuwa kukamilika kwa bandari hiyo mpya kutaongeza mapato ya Serikali na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri zaidi ya ushindani wa kikanda katika sekta ya bandari na usafirishaji wa majini.
Ziara ya Waziri Prof. Mbarawa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha miradi mikubwa ya kimkakati inatekelezwa kwa ufanisi, uwajibikaji na kwa kuzingatia malengo ya kukuza uchumi wa Taifa na kuboresha ustawi wa wananchi.


Baraza Kuu la Majadiliano (CJIC) la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) leo tarehe 18 Disemba 2025 limefanya Kikao cha Kaiwaida cha 58 kinachofanyika mjini morogoro.
Kikao hiko cha siku tatu kimeongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Claudio Mbena na kimelenga kujadili na kupitisha taarifa ya utekelezaji wa makubaliano ya kikao cha kawaida cha 57 cha Baraza kuu la Majaduliano CJIC kilichofanyika Septemba 11 na 12, 2025.
Pamoja na mambo mengine baraza hilo limempongeza Mkurugenzi Mkuu Mamalaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce M. Mbossa kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO.


Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepongezwa kwa ufanisi wa uhudumiaji wa shehena kwa haraka na ndani ya muda mfupi.
Kauli hiyo imetolewa Disemba 17 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Arusha mjini Mhe.Joseph Mkude alipotembelea banda la TPA katika Viwanja vya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) akiwa anamwakilisha Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Mb) katika kufunga Mkutano wa 18 wa tathmini ya utendaji wa sekta ya Uchukuzi ulienda sambamba na maonesho ya taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi na TAMISEMI uliofanyika kwa siku tatu kuanzia Disemba 15 hadi 17,2025.
Sambamba na kufunga Mkutano na Maonesho hayo, Mhe.Mkude alitoa tuzo kwa taasisi mbalimbali zilizopo chini ya Wizara hizo huku TPA ikipewa tuzo ya “heshima ya uongozi wa mfano, maono, kujitolea na utekelezaji wa Mkataba wa utendaji kazi kati ya taasisi na Wizara.
Katika mkutano huo na maonesho, Viongozi wa serikali, taasisi na sekta binafsi walipata fursa ya kutembelea banda la TPA kwa ajili ya kupata maelezo ya kina kuhusu shughuli za kibandari.


Wafanyakazi wa Bandari ya Mtwara wameshiriki katika semina ya mafunzo ya Ulinzi na Usalama wa Bandari (ISPS Code) yaliyofanyika tarehe 16 Disemba, 2025 Mkoani Mtwara.
Mafunzo hayo yameongozwa na Mkufunzi ambaye ni Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania Bw. Khalid Kitentya yamelenga kuwajengea uwezo na uelewa wa kina Wafanyakazi kuhusu taratibu, wajibu na mbinu bora za kuimarisha ulinzi na usalama wa Bandari kwa mujibu wa viwango vya Kimataifa vya ISPS Code.
Akifungua rasmi mafunzo hayo kwa niaba ya Meneja wa Bandari ya Mtwara, Afisa Utawala Mwandamizi Bi. Fassie O. Mushi amewahimiza wafanyakazi kushiriki kikamilifu na kuzingatia mafunzo hayo muhimu. Alisisitiza kuwa, matokeo chanya ya mafunzo hayo yatasaidia kuiweka Bandari katika hali ya usalama zaidi.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za Bandari ya Mtwara katika kuboresha usalama ili kuendana na viwango vya Kimataifa vya uendeshaji wa Bandari.


- TPA YAWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MWAKA 2024/25 JIJINI ARUSHA
- TPA YASHIRIKI KATIKA KIKAO CHA MKUTANO WA 18 WA TATHMINI YA UTENDAJI WA SEKTA YA UCHUKUZI JIJINI ARUSHA
- TPA YAPOKEA CHETI CHA PONGEZI KUTOKA CHUO CHA DMI KATIKA MAHAFALI
- TPA YAZINDUA MTAMBO MPYA WA REACH STACKER JIJINI DAR ES SALAAM
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"