Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe.Joel Arthur Nanauka ametembelea Banda la Bandari ya Mtwara katika maonesho yaliyoshirikisha wadau waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa zao la korosho.
Maonesho hayo yameambatana na Mbio za Korosho Marathon ambazo zimefanyika tarehe 29.11.2025. Mhe.Nanauka ameeleza kuridhishwa na taarifa za hali ya utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara kufuatia kuongezeka kwa uwezo wa kuhudumia shehena kutoka Tani milioni 1.7 kwa mwaka hadi kufikia zaidi ya Tani milioni 2.5 kwa mwaka.
Akiwasilisha taarifa hizo, Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara Bw. Mtunze Sudi ameeleza kuwa kwa sasa Bandari ya Mtwara imeimarisha zaidi huduma zake ambapo inahudumia shehena ya Mafuta ya transit ambayo yanasafirishwa kwenda nchi mbalimbali ikiwemo Malawi, Zambia, Rwanda, DRC na Burundi.


Timu za mabingwa wa jumla wa mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni binafsi nchini (SHIMMUTA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kama ilivyotarajiwa, zimeanza kibabe kutetea mataji yao katika mashindano yanayoendelea Mkoani Morogoro.
Mashindano hayo yaliyoanza wiki hii yalishuhudia timu ya Kandanda ya TPA ikiitembezea kichapo timu ya Chuo Kikuu Mzumbe kwa mabao 3 - 1, huku timu ya mpira wa kikapu ikiishiinda TRA kwa vikapu 52 - 25 na mechi iliyofuata ikaichabanga TRC vikapu 35 - 24.
Kwa upande wa Netiboli, timu ya TPA ambao ndio mabingwa watetezi imeifunga DIT 50 9 na BOT 52 - 10. Kwenye Mpira wa Wavu (Wanawake) timu ya TPA iliishinda NEMC kwa seti 2 - 0 na TANESCO kwa seti 2 -1.
Kwa upande wa mchezo wa kuvutana kwa Kamba,Timu ya TPA (wanaume) imecheza na timu za NIDA, NIT na SIDO na kushinda mechi zote kwa mivuto miwili kwa sufuri. Timu ya Wanawake nayo vile vile imeshinda michezo yake yote mitatu dhidi ya Mzinga,TSLB na MUHAS.


Bandari ya Tanga kwa mara ya kwanza imeandika historia baada ya kupokea Meli ya MVPARNIA yenye Makontena 463 kutoka Iran.
Akiongea mara baada ya kupokea meli hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dkt. Balozi Batilda Burian, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika bandari hiyo na matunda yake kuonekana.
“ Nampongeza Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono makubwa ya kuwekeza katika Bandari ya Tanga na leo hii tumeandika historia katika bandari hii kwa kupokea meli yenye Makontena mengi jambo ambalo halikuwahi kutokea huko nyuma kabla ya maboresho” Aliongeza Balozi Burian.
Aidha Balozi Burian alisema kuwa ujio wa meli hiyo katika Bandari ya Tanga kutoka Iran, ni fursa kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga na Mikoa mingine kufungua fursa za kibiashara baina ya Tanzania na Iran kwa kupitishia mizigo yao katika Bandari ya Tanga.Katika hatua nyingine Balozi Burian aliahidi kuendelea kujenga ushirikiano wa kibiashara na Iran kwa kutumia bandari ya Tanga ili kuhudumia nchi za Afrika Mashariki na nchi za Ukanda wa SADC.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba alisema kuwa ujio wa meli hiyo katika Bandari ya Tanga ni fahari kwa wananchi kwani uchumi wa Tanzania utazidi kukua na fursa za kibiashara zitazidi kufunguka zaidi.awali akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa, Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Peter Millanzi alisema kuwa kwa muda mrefu Bandari ya Tanga ilikuwa inapokea meli ndogo ndogo “Feeder Vessels “ kutoka Bandari za nchi jirani sababu bandari ilikuwa haina uwezo wa kupokea meli kubwa za makontena.
Hata hivyo kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika kwa sasa Bandari ya Tanga ina uwezo wa kupokea meli kubwa na sasa historia imeandikwa ya kupokea meli kubwa za makontena kutoka moja kwa moja nchini Iran.Meli hiyo yenye urefu wa mita 174 na kina cha mita 10.3 imetia nanga katika Bandari ya Tanga ikiwa na makontena 463, ambapo makontena 261 yakiwa ni ya Tanzania na makontena 182 yakwenda katika nchi za za Rwanda, Zambia, Malawi na Uganda.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof.Godius Kahyarara ameongoza kikao cha 33 cha Kamati ya Maboresho ya Bandari (PIC) kilichofanyika Novemba 28,2025 Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam.
Kikao cha Kamati hiyo ya Maboresho ya Bandari (Port Improvement Committee) hukutanisha Taasisi na Wadau mbalimbali wanaotumia bandari kikilenga kujadili utekelezaji wa changamoto mbalimbali katika sekta ya Uchukuzi na kuzipatia ufumbuzi.


Bandari ya Mtwara imeendelea kupokea Wafanyabiashara mbalimbali wenye nia ya kuitumia Bandari hiyo kupitisha shehena zao, ambapo Novemba 28,2025, Uongozi wa Kampuni ya SOIL SOLUTIONS wakiongozwa na Meneja wa Miradi Bw. Ashok Shetty, umefanya ziara katika Bandari hiyo kwa lengo la kujiridhisha na uwezo wa Bandari katika kuhudumia shehena.
Bw. Ashok ameeleza kuridhishwa na Bandari ya Mtwara ambapo amefafanua kuwa mwezi Januari 2026 wanatarajia kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa Kiwanda kikubwa cha Mbolea ya UREA Mkoani Mtwara. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha Tani 1,750 kwa siku ambapo asilimia 80 ya uzalishaji huo utasafirishwa kwenda katika masoko mbalimbali ya kimataifa.
Vilevile, ameeleza kuwa wakati wa kuanza kwa mradi wa ujenzi, wanatarajia kuitumia Bandari ya Mtwara kupitishia vifaa vya ujenzi kiasi cha zaidi ya Tani 20,000.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara Bw. Mtunze Sudi ameeleza kuwa Bandari ina uwezo mkubwa na ipo tayari kuhudumia shehena hizo kufuatia uwepo wa miundombinu wezeshi, vitendea kazi vya kisasa na rasilimaliwatu wa kutosha.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"