Baraza la Wafanyakazi (WC) la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kituo cha Makao Makuu, limefanya kikao cha (38) kilichofanyika mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Kikao hicho cha moja kilitanguliwa na Kikao cha Kamati ya Utendaji kilichokaa tarehe 12 na 13 Novemba 2025 kufuatiwa na Kikao cha Baraza kilichofanyika tarehe 14 Novemba 2025 kilicholenga kupokea na kujadili taarifa ya Utendaji kazi na taarifa ya utekelezaji wa mpango wa Bajeti kwa mwaka 2024/2025 na nusu Mwaka (Januari - Juni 2025)
Baraza hilo limeongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mha. Dkt. Baraka R. Mdima.


Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Salehe Mbega, ametoa pongezi kwa Menejimenti na Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari (DOWUTA) kituo cha Tanga kwa namna wanavyoshirikiana kuhakikisha Bandari ya Tanga inafikia malengo yaliyowekwa.
Bw. Mbega alitoa pongezi hizo alipokuwa anafunga Kikao cha 70 cha Baraza la Majadiliano la kituo hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano katika Jengo la Bandari (Bandari House).
“ Nawapongeza Menejimenti na Upande wa wawakilishi wa Chama (DOWUTA) kwa namna mnavyoshirikiana na kuwa na lengo moja kuhakikisha bandari yetu inafanyakazi vizuri”.
Alisema Mbega Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari (DOWUTA), Bw. Aliko Mwakipagala alimuhakikishia Meneja huyo kuendelea kuchapa kazi na kupokea maelekezo mbalimbali yatakayokuwa yanatolewa ili kuongeza tija na ufanisi.
Katika kikao hicho hoja mbalimbali zilijadiliwa na changamoto mbalimbali zilitafutiwa ufumbuzi ili kuhakikisha shughuli za kibandari zinafanyika kwa ufanisi.


Bandari ya Mtwara imefanya kikao chake cha thelathini na nane (38) cha Baraza la Wafanyakazi, tarehe 13 Novemba 2025 Mkoani Lindi.
Kikao hicho kimeongozwa na Meneja wa Bandari ya Mtwara Bw. Ferdinand S. Nyathi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo.
Lengo kuu la kikao hicho ni kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara ikiwemo mipango na mikakati ya maendeleo ya Bandari, mapato na matumizi, uhudumiaji wa shehena na meli pamoja na masuala mengine muhimu ya kiutawala na kiutendaji.
Kikao hicho kimefanyika kwa mafanikio makubwa ambapo wajumbe walipata fursa ya kujadili na kutoa maoni yenye lengo la kuboresha zaidi huduma na ufanisi wa Bandari ya Mtwara.
Kupitia majadiliano hayo, Baraza limeazimia kuendelea kushirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa mikakati inayolenga kuinua tija na kuongeza mchango wa Bandari ya Mtwara katika kukuza uchumi wa Taifa.


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Kenan Sawala, ameeleza kuridhishwa kwake na maandalizi makubwa yaliyofanywa na wadau wote wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa zao la Korosho.
Mhe. Kanali Sawala ametoa kauli hiyo tarehe 10 Novemba 2025, baada ya kufanya ziara ya kukagua maeneo yatakayotumika kufungashia shehena ya korosho (stuffing areas) pamoja na kutembelea Bandari ya Mtwara.
Amesema ana imani kubwa kuwa korosho zote zinazolimwa mikoa ya Kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, zinazokadiriwa kufikia takriban tani 700,000 msimu wa 2025/2026 zitasafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kanali Sawala aliambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Abdallah Mussa Mwaipaya, Menejimenti ya Bandari ya Mtwara, pamoja na viongozi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT).
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand Nyathi, alibainisha kuwa bandari imejipanga kikamilifu kutoa huduma bora kwa msimu huu wa usafirishaji wa korosho kwa kuwa na miundombinu imara, vifaa vya kutosha, na rasilimali watu wenye weledi.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, ametoa wito kwa Wafanyakazi na Wananchi wa Mkoa huo, kulinda miundombinu ya Bandari ya Tanga kwani ni tunu ya Mkoa huo kiuchumi.
Balozi Dkt. Burian ametoa wito huo, wakati wa mapokezi ya baada ya Meli ya MV ELISAR iliyotia nanga bandarini hapo ikiwa na Shehena Tani 33,000 ( Elfu thelathini na tatu) ya mizigo mchanganyiko.“Ujio wa meli hii ni matunda ya uwekezaji uliofanyika katika Bandari ya Tanga, kwahiyo sisi kama watendaji na wananchi kwa jumla tuone ni tunu katika Mkoa wetu hivyo, hatuna budi kutunza miundombinu ya bandari yetu” Alisema Balozi Burian.
Aidha Balozi Burian alisema kuwa Bandari ya Tanga licha ya kuiletea sifa Tanzania pia imekuwa ikinufaisha wananchi wa Tanga mmoja baada ya mwingine kuanzia kwenye ajira mpaka kwenye mzunguko wa pesa kwa wananchi.Pia Balozi Dkt. Burian amewataka wadau mbalimbali kuendelea kuitumia bandari hiyo ambayo inazidi kusogeza huduma zake baada ya hivi karibuni kuzindua reli ya mizigo kutoka bandarini hapo na kuunganisha na reli ya kati kupitia Ruvu kwenda Mikoa ya Magharibi na nchi jirani.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Salehe Mbega, alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa Bandari ya Tanga imejipanga vyema katika kuihudumia meli hiyo kuanzia wafanyakazi na vitendea kazi vya kisasa.
Meli hiyo yenye urefu wa mita 187 imeletwa na Kampuni ya Seafront Shipping Services LTD na imetia nanga bandarini hapo ikitokea nchini China ikiwa imebeba mizigo mchanganyiko kama Magari na Mitambo mbalimbali ya viwandani.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"