Michezo ya 18 ya Bandari “InterPorts Games 2025” imefungwa rasmi leo mjini Morogoro, huku Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw.Plasduce Mbossa, akisisiatiza umuhimu wa watumishi wote wa sekta ya bandari kushiriki kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Maelekezo hayo ya Mkurugenzi Mkuu yametolewa katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TPA, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo, Bw. Mbarakiwa Masinga.
Bandari ya Dar es Salaam imeibuka Mshindi wa jumla wa Michezo hiyo Mwaka 2025 ikiwa ni mara ya tatu mfululizo huku ikinyakua jumla ya vikombe 13 kati ya vikombe vilivyokuwa vinawaniwa na jumla ya timu zilizoshiriki Mashindano hayo.
Bandari ya Dar ea Salaam imetwaa ubingwa wa Mpira wa Wavu kwa Wanawake na Wanaume, na pia ikiongoza upande wa Riadha mita 1500 na kufuatiwa na Bandari ya Tanga na DP World.
Kwa upande kwa Kandanda timu ya Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) ilinyakua ubingwa baada ya kuilaza Bandari ya Dar es Salaam 1 - 0 katika mchezo wa fainali,huku nafasi ya ushindi wa tatu ikinyakuliwa na Makao Makuu DP World baada ya kuifunga timu ya DP World magoli 4 - 3.
Kwenye Mpira wa Netiboli Timu ya Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) imekuwa mshindi kwa tofauti ya magoli 16 dhidi ya timu ya Bandari ya Dar es Salaam huku Bandari ya Tanga ikitwaa ubingwa wa mchezo wa mpira wa kikapu.
Kwa upande wa mpira wa Wavu Wanawake bingwa ameibuka Bandari ya Dar es Salaam akifuatiwa na Bandari za Mtwara na Tanga.Katika mchezo wa kamba wanaume bingwa ni Bandari ya Tanga,mshindi wa pili ni Shirika la Bandari Zanzibar na mshindi wa tatu ni Bandari ya Dar es Salaam.
Kufuatia matokeo hayo yalishirkisha timu na wachezaji kutoka Makao Makuu ya TPA, Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Maziwa, DP World, TACOSHIL na Shirika ka Bandari Zanzibar, Mkurigenzi Mkuu ameipongeza Kamati ya Maandalizi kwa kufanikisha michezo hiyo kwa nidhamu na uadilifu.


Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Watumishi wote wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) tunaungana na Wateja, Wadau na Umma kwa ujumla kuadhimisha kumbukizi ya Siku ya Nyerere.
Tunaendelea kuuenzi daima mchango wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika maendeleo ya Taifa letu, kwa kuendelea kuboresha zaidi huduma za Kibandari ili kuongeza mchango wa Taasisi hii katika maendeleo ya Taifa na Nchi zinazohudumiwa na Bandari zetu.
#tpa#sikuyanyerere#nyerereday#kumbukiziyamiaka26
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania IGP Mstaafu Mhe. Balozi Ernest J. Mangu ameongoza wajumbe wa Bodi hiyo katika ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa, tarehe 10 Oktoba 2025.
Ziara hiyo ilihusisha kutembelea miundombinu ya Bandari na kupata taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa Bandari hiyo ya kisasa ambao unatekelezwa na Kampuni ya CHEC ya Nchini China ili kushuhudia hatua na hali halisi ya mradi huo ilivyo kwa sasa.
Mhe. Balozi Mangu alieleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa Bandari hiyo ambayo inatarajiwa kuchakata zaidi ya Tani 60,000 za shehena ya samaki kwa mwaka mara itakapokamilika na kuanza kazi.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Kampuni ya CHEC Bw. Douglas Semwenda ameeleza kuwa, mradi huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 266 ulianza kutekelezwa mwezi Septemba, 2023 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 88 ya utekelezaji wake na unatarajiwa kukamilika rasmi mwezi Februari, 2026.


Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja “Customer Service Week” Bandari ya Tanga Kitengo cha Tehama kimeendelea kutoa huduma bora kwa wateja kupitia mifumo.
Akizungumza juu ya maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila mwaka mwezi Oktoba, Afisa Mwandamizi Kitengo cha Tehama Bandari ya Tanga Bw. Johanes Rwezaula alisema kuwa katika kuwezesha utoaji wa huduma bora kwa wateja miundombinu ya mawasiliano katika bandari hiyo yameimarika.
“Miundombinu ya mawasiliano imeboreshwa na mifumo imeimarika hakuna tena changamoto za mara kwa mara za kukatika kwa mtandao jambo ambalo limesaidia kurahisisha utendaji kazi katika utoaji wa mizigo na upatikanaji wa taarifa” Aliongeza Rwezaula.
Aidha pia Rwezaula alisema kuwa mifumo inayotumika bandarini ya ITOS na POAS ambayo imeunganishwa na mifumo ya Taasisi zingine kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama TANCIS na Wizara ya Fedha GePG imesaidia utendaji kazi bandarini, hivyo aliwataka wateja waendelee kufurahia huduma zinazotolewa bandarini hapo.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) IGP Mstaafu Mhe.Balozi Ernest J. Mangu, ameongoza wajumbe wa Bodi hiyo katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara, tarehe 9 Oktoba 2025.
Ziara hiyo ilihusisha kutembelea Bandari hiyo na kupata taarifa za utendaji kazi wake, pamoja na kutembelea Mradi wa Usanifu na Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao ili kushuhudia maendeleo ya utekelezaji wake.
Mhe. Balozi Mangu alieleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Mradi huo, ambao unatarajiwa kuhudumia tani milioni 2.5 za shehena kwa mwaka utakapokamilika.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mha. Dkt. Baraka Mdima, ameeleza kuwa TPA itaendelea kuzisimamia na kuziendeleza Bandari zote nchini, ikiwemo Bandari ya Mtwara, ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya huduma za bandari na kuiwezesha sekta ya bandari kutoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Akieleza matarajio yaliyopo, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand Nyathi, amesema kuwa mwelekeo na mtazamo wa kimasoko kwa sasa ni chanya, kwa kuwa Bandari imeanza kuhudumia shehena ya mafuta yanayosafirishwa kwenda nchi jirani za Zambia na Malawi, hatua ambayo inazidi kufungua milango ya Bandari kwa kuhudumia shehena zaidi katika nchi hizo.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"