Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekuwa ikichangia maendeleo ya Uchumi wa Buluu kupitia uendelezaji na ujenzi wa Bandari za mwambao wa Bahari na maziwa makuu nchini.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 11, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara, wakati akifunga Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Uchumi wa Buluu 2025, lililofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake Prof. Kahyarara amesema, Serikali kupitia TPA imefanya maboresho katika bandari zake za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara pamoja na za Ziwa Nyasa, Victoria na Tanganyika, ili kuchochea maendeleo ya Uchumi wa Buluu.
Aidha Prof.Kahyarara amesema, Bandari zilizoko kwenye maziwa zinaunganisha nchi yetu na nchi zisizo na bahari kupitia usafirishaji wa shehena kwa njia ya maji.
Amesema kwa maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, Bandari hiyo inaenda kuwa kivutio zaidi na chaguo kwa Wateja, katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.




Baraza kuu la Majadiliano (CJIC) la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) limefanya kikao cha kawaida cha Hamsini na Saba (57) kinachofanyika mjini Morogoro.
Kikao hiko kimelenga kupitia na kuthibitisha Utekelezaji wa Makubaliano ya Kikao cha kawaida cha Hamsini na sita (56) kilichofanyika Disemba 2024.
Pamoja na mambo mengine, Baraza hilo limewaaga wajumbe wake ambao ni Afisa Mwandamizi Bandari ya Kyela Bw. Florian Mloka na Katibu wa DOWUTA Tawi la Dar es Salaam Bw. Hassan Ahmed kwa kuhitimisha muda wa wao wa utumishi kisheria katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).




Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na waendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL), wameendesha kampeni ya kimasoko katika mji wa Lubumbashi, DR Congo.
Ziara hiyo ililenga kusikiliza changamoto za wateja na wadau wa biashara, pamoja na kuwasilisha maboresho makubwa yaliyofanywa katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Kigoma.
Akifungua mkutano huo, Konseli Mkuu wa Tanzania mjini Lubumbashi, Bw. Magubilo Muroba, alipongeza ushirikiano kati ya bandari za Tanzania na wafanyabiashara wa DR Congo, uliosababisha ongezeko la mizigo kwa asilimia 43 kutoka tani milioni 4.1 mwaka 2023/24 hadi milioni 5.9 mwaka 2024/25.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Josephat Lukindo, alisisitiza dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kutoa huduma za kisasa. Ushirikiano wa TPA na waendeshaji wake, ukiungwa mkono na uwekezaji wa mitambo ya kisasa, umefanya muda wa kuhudumia meli za makasha kupungua hadi wastani wa siku tatu.
Mbali na mkutano, ujumbe huo ulitembelea kampuni kubwa za usafirishaji ikiwemo Impala Cargo Terminal na Conexas Terminal, ambazo zote ziliridhishwa na huduma zitolewazo na kuahidi kuendeleza ushirikiano na bandari za Tanzania.


Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inashiriki Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Uchumi wa Buluu 2025, linaloenda sambamba na maonesho ya shughuli zinazofanywa na Taasisi shiriki, na linafanyika kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo linaloenda na kauli mbiu ya “Bahari Yetu,Fursa Yetu, Wajibu Wetu: Kuanzia 2021 hadi 2025”, limefunguliwa Septemba 10, 2025 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Mhawi.
Kwa upande wa Maonesho, Banda la TPA limekuwa kivutio kwa Wadau mbalimbali wa Uchumi wa Buluu kutembelea kwa ajili ya kupata maelezo kuhusu majukumu ya Mamlaka na shughuli mbalimbali za utekelezaji Bandarini.




Balozi wa Urusi hapa nchini Mhe. Andrey Avetisyan, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kuendelea kuiboresha Bandari ya Mtwara, inayoendelea kutoa huduma bora na za ufanisi.
Balozi Avetisyan, ametoa pongezi hizo, tarehe 8 Septemba, 2025 alipofanya ziara ya kutembelea Bandari ya Mtwara, ambapo ameongozana na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Patrick Kenan Sawala pamoja viongozi mbalimbali wa ngazi ya Mkoa.
Amesema pia ameridhishwa na utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara, na kueleza kubaini fursa mbalimbali zilizopo katika Bandari hiyo, ambazo zikitumiwa vizuri zitaleta maendeleo na ongezeko la mapato zaidi.
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Mtwara Bw. Ferdinand Nyathi, ameelezea hali ya utendaji kazi wa Bandari hiyo kuwa umeimarika zaidi , kufuatia maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Serikali ambayo yameongeza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma.




- BARAZA KUU LA WAFANYAKAZI WA TPA LIMEFANYA KIKAO CHA THELATHINI NA NANE (38) JIJINI MOROGORO
- MSAJILI WA HAZINA, BW. NEHEMIA MCHECHU AFANYA ZIARA KATIKA BANDARI YA TANGA
- KAMATI YA MABORESHO YA BANDARI IMEKUTANA KATIKA KIKAO CHAKE CHA 33
- CEO'S FORUM 2025 KATIKA KITUO CHA MIKUTANO CHA KIMATAIFA CHA ARUSHA
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"