Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Dkt.Ladislaus Chang’a ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa ufanisi na uweledi katika kuhudumia Shehena.
Dkt.Chang’a ametoa kauli hiyo Agosti 04,2025 alipotembelea banda la TPA lililopo katika Viwanja vya Nzuguni Dodoma yanakofanyika Maonesho ya Wakulima (Nanenane)
Banda la TPA limekuwa kivutio katika Maonesho hayo yanayotarajiwa kufikia kilele Agosti 08, 2025 kwa watu wa rika tofauti kutembelea kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yahusuyo sekta ya Uchukuzi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Julai 31,2025, ameweka jiwe la msingi la uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Vigwaza, Kibaha Mkoa wa Pwani.
Bandari hiyo ya kitaifa na kikanda imejengwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 502 ambapo kati ya hizo hekta 120 zimesafishwa na hekta tano zimejengwa kwa kiwango cha zege zikiwa ndani ya eneo la hekta 60 zilizozungushiwa uzio wenye urefu wa kilometa 2.96.
Bandari kavu ya Kwala inatarajiwa kuhudumia na kuhifadhi shehena ya makasha 3500 kwa siku na idadi ya makasha zaidi ya 300,000 kwa mwaka ikiwa ni takribani Asilimia 30 ya Makasha yote yanayopita katika Bandari ya Dar es Salaam.
Bandari hiyo itahudumia pia nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC), Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda na Uganda, ambapo nchi zote hizo zimepatiwa maeneo ndani ya Bandari Kavu hiyo ya Kwala.



Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetia saini makubaliano ya taratibu za uendeshaji wa Kawaida (SOPs) zilizotayarishwa kwa ajili ya uhamishaji, uhifadhi na usafirishaji wa shehena kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Bandari Kavu ya Kwala, iliyopo Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Hafla hiyo ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika Julai 28,2025 Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam, ikihusisha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Reli Tanzania (TRC) na waendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Kampuni za DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL).
Akizungumza mara baada ya kusainiwa makubaliano hayo yanayoenda kuifungua Bandari ya Dar esSalaam, Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw.Plasduce Mbossa, amesema taratibu hizi zimetayarishwa kwa pamoja na kila Taasisi imeonyeshwa nini inachotakiwa kufanya katika mchakato mzima wa Uchukuzi wa shehena kutoka bandari ya Dar es Salaam.
Aidha Bw.Mbossa amesema makubaliano hayo yatapunguza muda wa uondoshaji mzigo bandarini, msongamano wa magari makubwa, kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uhudumiaji wa shehena.
Naye Mkuu wa Idara ya Utekelezaji wa TEAGTL Bw.Laksiri Noni amepongeza uamuzi wa kushirikisha wadau wote wanaohusika katika mnyororo mzima wa Uchukuzi wa shehena katika makubaliano hayo.






Timu za Mpira wa Wavu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Wanaume na Wanawake zimeshiriki ufunguzi wa Ligi ya Mpira wa Wavu Taifa -Tanzania Volleyball National League (TVNL) uliofanyika katika viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam.
Kocha wa timu hizo Bw.Willy Barton amesema kuwa vikosi vyake vipo tayari kwa ligi hiyo na kuwahakikishia Menejimenti ya TPA, Mashabiki na Wadau, ushindi katika mechi zote na hatimaye kunyakuwa ubingwa wa michuano hiyo.
Aidha Timu ya Mpira wa wavu wanawake ya TPA, tarehe 26 Julai 2025 itaingia dimbani dhidi ya Jeshi Stars katika mchezo utakaochezwa katika viwanja vya Mwembe Yanga Jijini Dar es Salaam.
Ligi ya Mpira wa Wavu Taifa imeandaliwa na Chama cha mpira wa Wavu Tanzania (TVF) ikishirikisha timu 14 kwa Wanaume na kwa upande wa Wanawake ni timu 7 ambapo ligi hiyo itaanza rasmi kuchezwa tarehe 26 Julai hadi Agosti 1, 2025.


Serikali imetoa wito kwa wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wote wa sekta ya usafirishaji kushiriki katika hafla ya uzinduzi wa Bandari kavu ya Kwala iliyopo Vigwaza Mkoa wa Pwani, unaotarajiwa kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 31,2025.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Julai 25,2025, Makao makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, amesema hafla ya uzinduzi wa Bandari kavu ya Kwala ni ya kitaifa na itaenda sambamba na uzinduzi wa usafirishaji wa Shehena kwa treni ya SGR Kati ya Dar es Salaam na Dodoma pamoja na upokeaji wa mabehewa ya mizigo ya Treni ya Kawaida (MGR) ambapo mabehewa 50 ni mapya na mabehewa 20 yaliyokarabatiwa kwa ufadhili wa Wakala wa Uwezeshaji wa Ushoroba wa Kati (CCTTFA).
“Rais wetu mpendwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, atazindua rasmi bandari hii muhimu kwa taifa letu, pamoja na huduma za kisasa za usafirishaji wa mizigo. Huu ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha uchumi wa viwanda kupitia miundombinu madhubuti ya uchukuzi,” amesema Mhe. Waziri Prof. Mbarawa.
Mhe. Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa bandari hiyo imejengwa kwa lengo mahsusi la kuongeza ufanisi katika kushughulikia shehena zinazowasili katika Bandari ya Dar es Salaam hasa baada ya maboresho makubwa yaliyofanyika kwenye bandari hiyo.
“Kupitia Bandari Kavu ya Kwala, tunategemea ufanisi mkubwa katika kuhudumia shehena. Hii itasaidia kuongeza mapato ya Serikali kutokana na huduma zitolewazo katika Bandari ya Dar es Salaam na Kwala, huku tukipunguza gharama za uendeshaji kwa wafanyabiashara na kuwa kivutio kikubwa kwao kutumia Bandari ya Dar,” amesema Waziri Mbarawa.
Mhe. Waziri ameongeza kuwa hatua hii pia itaongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, hasa ikizingatiwa kwamba nchi jirani nazo zinawekeza kwa kasi katika bandari zao.
Faida nyingine zilizotajwa na Mhe. Waziri ni pamoja na kupungua kwa msongamano wa magari barabarani hususan Barabara ya Mandela na maeneo ya karibu na Bandari ya Dar es Salaam, kuimarika kwa usalama barabarani na kupungua kwa gharama za matengenezo ya barabara zinazoharibiwa na malori ya mizigo.
Aidha Mhe. Waziri amesisitiza kuwa ujio wa Bandari Kavu ya Kwala umeanza kuleta matumaini kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani, ambapo tayari kunashuhudiwa ongezeko la shughuli za kiuchumi, ajira kwa wananchi wa eneo hilo na matarajio ya uwekezaji wa viwanda kutokana na uwepo wa miundombinu madhubuti ya usafirishaji kuelekea Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri Prof. Mbarawa pia amewahimiza
wadau hao kuchangamkia fursa zitakazopatikana kupitia huduma za gharama nafuu na ufanisi wa muda mfupi zinazotolewa na Bandari Kavu ya Kwala, treni za kisasa za SGR na mabehewa mapya ya MGR.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) Bw. Plasduce Mbossa, amesema ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam, huku ikiendelea kuboresha na kupanua miundombinu ya bandari nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi na ushindani wa kitaifa na kikanda.
“ Bandari Kavu ya Kwala ni jitihada na mkakati madhubuti wa kitaifa unaolenga kuondoa changamoto sugu ya msongamano wa mizigo Bandarini na maeneo ya barabara ya Mandela Jijini Dar es Salaam.” amesema Bw. Mbossa.


- MENJIMENTI YA TPA NA TRC YATEMBELEA BANDARI KAVU YA KWALA IKIWA NI UKAGUZI WAMAADALIZI YA UZINDUZI NA MHE. RAIS DKT SAMIA SULUHU HASSAN
- KIKAO CHA TATU (3) BARAZA LA MAJADILIANO BANDARI YA DAR ES SALAAM
- MAOFISA WA KIKOSI MAALUM CHA KUZUIA NA KUPAMBANA NA MAGENDO ZANZIBAR KMKM WAFANYA ZIARA YA KIMAFUNZO BANDARI YA DAR ES SALAAM
- HAFLA YA UZINDUZI WA BANDARI KAVU YA KWALA
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"