Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari (DOWUTA) Tawi la Bandari ya Dar es Salaam wamemchagua Bw. Mashaka Karume kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho, huku Bw. Eliakimu Maluli akishinda nafasi ya Katibu katika Uchaguzi Mkuu wa DOWUTA uliofanyika tarehe 3 Februari 2026 katika viwanja vya Zimamoto na Usalama Bandari ya Dar es Salaam.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliokuwa sambamba na uchaguzi wa viongozi, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed G. Abed, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, aliipongeza DOWUTA kwa kudumisha utulivu na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi, hali inayochangia kuboreshwa kwa maslahi yao na kuongeza ufanisi kazini.
Bw. Abed alisema kuwa utulivu na moyo wa kujituma wa wafanyakazi, kwa kiasi kikubwa, umechagizwa na mchango wa DOWUTA, hali iliyopelekea kuongezeka kwa ufanisi wa kazi bandarini. Alieleza kuwa katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka wa fedha 2025/2026, Bandari ya Dar es Salaam imehudumia tani milioni 16.7, ongezeko la tani milioni 3.9 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Aidha, alisema kuwa kwa kasi hiyo ya utendaji, Bandari ya Dar es Salaam inatarajiwa kuhudumia zaidi ya tani milioni 32 ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2025/2026, kiwango kinachozidi lengo la tani milioni 27.7, mafanikio aliyoyataja kuwa ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Menejimenti na DOWUTA.
Katika nafasi nyingine za uongozi, Bi. Sharifa Yahya amechaguliwa kuwa Mweka Hazina, Bw. Shabani Godigodi akishinda nafasi ya Mwakilishi wa Watu Wenye Uhitaji Maalum, huku Bw. David Mtambazi na Bi. Tunu Masenga wakishinda nafasi za Uwakilishi wa Vijana Wanaume na Wanawake mtawalia.
Kwa upande wa Wajumbe Wanawake waliochaguliwa ni Bi. Dainess J. Binemukama, Bi. Theopista W. Millinga, Bi. Chema Y. Mwaduga, Tatu Mandao na Dr. Bertha O. Mushi, huku wajumbe wa idara mbalimbali wakichaguliwa kuwakilisha sekta zao ikiwemo Uhandisi, Utekelezaji, Ulinzi na Zimamoto, Marini, Bandari Ndogo, Rasilimali Watu na Utawala pamoja na Usaidizi wa Biashara, Ugavi, Fedha na Mapato.


Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (MNEC) Comrade Richard Kasesera,tarehe 3 Februari, 2026 ameongoza ujumbe wa Wanachama wa CCM katika ziara ya kikazi ya kutembelea Bandari ya Mtwara.
Lengo la ziara hiyo ni kujionea maendeleo ya Bandari ya Mtwara baada ya maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kupata taarifa ya utendaji kazi wa Bandari.
Katika ziara hiyo, Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara Kapt. Paul Muchwampaka alieleza masuala mbalimbali ikiwemo mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto kadhaa zinazoikabili Bandari ya Mtwara.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Comrade Kasesera alipongeza utendaji kazi mzuri wa Bandari ya Mtwara ikiwa ni pamoja na uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena. Aidha, alieleza kuwa atawasilisha katika ngazi za juu masuala mbalimbali ikiwemo changamoto zilizopo ili zitafutiwe ufumbuzi wa haraka kwa lengo la kuendelea kuimarisha ufanisi na mchango wa Bandari ya Mtwara katika maendeleo ya Taifa.
Maafisa wanafunzi na Wakufunzi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutoka Chuo cha Mafunzo ya Kikosi Maalum kilichopo Sangasanga Wilaya ya Morogoro leo tarehe 3 februari 2026 wametembelea Bandari ya Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wamejifunza shughuli za Bandari pamoja na namna TPA ilivyojidhatiti na utayari wake katika kupambana na hatari za kiusalama katika Bandari zake hususan Bandari ya Dar es Salaam ambalo ni langu kuu la Biashara kitaifa na kimataifa.
Ziara hiyo imeongozwa na Meneja Ulinzi na Usalama Bw. Said J. Mollel Kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, amewataka watumishi wapya wa taasisi hiyo kuweka maslahi ya umma mbele ya maslahi binafsi na kuutumikia umma kwa uadilifu, uwazi na uwajibikaji ili kulinda imani ya wananchi kwa Serikali.
Akizungumza wakati wa kufungua kozi ya awali ya mafunzo kwa watumishi wapya (Induction Course) iliyofanyika Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam, tarehe 2 Februari,2026, Bw. Mbossa amesema Serikali inawatazamia watumishi wa umma kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya ndani ya taasisi zao na katika jamii kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa utumishi wa umma si ajira ya kawaida, bali ni wito wa kulitumikia taifa kwa uaminifu na uzalendo wa dhati, akiwahimiza watumishi wapya kuzingatia maadili ya kazi, kufanya kazi kwa weledi na kujenga utamaduni wa uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Kumbukeni kuwa imani ya wananchi kwa Serikali hujengwa au hubomolewa kupitia mwenendo wa watumishi wake,” alisema Bw. Mbossa, akionya dhidi ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha taswira ya taasisi na utumishi wa umma kwa ujumla.
Aidha, aliwahimiza watumishi wapya kutumia mafunzo waliyoyapata kama msingi wa kujenga taaluma zao, wakizingatia misingi ya uadilifu, weledi na uzalendo, sambamba na kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto badala ya kuwa chanzo cha matatizo.
Akihitimisha hotuba yake, Mkurugenzi Mkuu aliwatakia watumishi wapya mafunzo mema na safari njema katika utumishi wa umma, akisisitiza umuhimu wa kulinda heshima ya taasisi na Taifa kwa ujumla.
Kozi hiyo ya “induction” inalenga kuwaandaa watumishi wapya wa TPA kwa kuwajengea uelewa wa majukumu ya taasisi, misingi ya utumishi wa umma, maadili ya kazi na matarajio ya Serikali katika kuboresha ufanisi wa bandari na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.



Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari (DOWUTA) tawi la Makao Makuu, kimekamilisha mchakato wa Uchaguzi wa nafasi mbalimbali za chama hicho Januari 30,2024.
Katika uchaguzi huo uliokuwa na hamasa kubwa tofauti na miaka iliyopita,ambapo mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti ni Bw.Felician Hasunga na Bw. Isaac Mtamba akiibuka mshindi katika nafasi ya Katibu Mkuu.
Nafasi zingine zilizokuwa zinagombaniwa ni nafasi ya Uwakilishi wa Vijana wanaume ambapo Bw. Shamte Luwali na Bw. Omary Khalid walifungana kwa kulingana idadi ya kura na hivyo uchaguzi wa nafasi hiyo itarudiwa, huku kwa upande wa Vijana wanawake mshindi ni Bi. Hilda Shundi.
Nafasi tano Wajumbe wanawake washindi ni Bi. Irene Mmari, Bi. Mary Mahinya, Bi. Queen Chiwanga, Bi. Caroline Urio na Bi. Mariam Namota.
Washindi wa nafasi za uwakilishi wa idara ni Bw. Zubeir Sungura, Bw. Aloyce Kakusa, Bi. Esther Mchomvu, Bw. Calist Nyaki, Bw. Atufigwegwe Mwanjala, Bw. Mutasa na nafasi ya mweka hazina wa chama imechukuliwa na Bw. Adili Mindolo.



EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"