Na Mwandishi Wetu
Ili kuendana na malengo ya Uchumi wa Bluu na Bandari ya Kijani (Blue Economy and Green Port), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeeleza hatua madhubuti inazochukua kuhakikisha kuwa shughuli za kibandari haziathiri mazingira.
Akizungumza wakati wa Kongamano na Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STICE), yanayoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dkt. Olivary John kutoka Chuo cha Bandari alieleza kuwa TPA imechukua hatua tano muhimu kudhibiti uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibandari.
Kwa mujibu wa Dkt. Olivary, hatua hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa Sera ya Usimamizi wa Mazingira ya TPA, ambayo inatoa mwongozo wa kulinda na kuhifadhi mazingira katika shughuli za bandari. Hatua nyingine ni uwekaji wa vitunza taka katika maeneo mbalimbali ya bandari ili kuhakikisha taka zinakusanywa na kusimamiwa ipasavyo.
Aidha, TPA imeimarisha juhudi za kudhibiti uzalishaji wa taka, ikiwemo kupunguza taka zinazozalishwa kupitia mbinu endelevu. Pia, mamlaka hiyo inazingatia mfumo wa utunzaji wa mazingira kulingana na kanuni za ISO, kuhakikisha bandari zake zinakidhi viwango vya kimataifa vya mazingira.
Hatua ya tano, kwa mujibu wa Dkt. Olivary, ni utunzaji wa bahari na upunguzaji wa uchafuzi wa mazingira kwa kuondoa taka laini na ngumu katika maeneo ya bahari, ili kuhifadhi usafi na uhai wa viumbe wa majini.
Hatua hizi zinathibitisha dhamira ya TPA katika kufanikisha maendeleo endelevu kupitia ulinzi wa mazingira na kuhakikisha bandari zake zinachangia uchumi wa taifa bila kuathiri mazingira.
Na Mwandishi Wetu
Mpango wa uboreshaji miundombinu katika Bandari ya Mtwara unaotekelezwa kupitia Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, umeongeza ufanisi ambapo zaidi ya tani 100,000 za korosho zimesafirishwa katika msimu huu wa zao hilo.
Mafanikio hayo yamepatikana baada ya kuongezwa vifaa vya kupakia na kushusha mizigo, hivyo kuchangia ongezeko la idadi ya meli zinazotia nanga kwenye bandari hiyo hali inayotajwa kuchochea zaidi uchumi katika ukanda wa kusini.
Akizungumza mkoani Mtwara wakati wa ziara ya kukagua maboresho katika bandari hiyo, Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, alisema serikali inatekeleza mkakati huo wenye lengo la kukuza uchumi na kufungua fursa za ajira kwa wananchi.
"Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuweka msukumo kwenye usimamizi na ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya uchukuzi na ndiyo sababu meli zimeanza kuja kwa wingi," alieleza.
Profesa Mbarawa alibainisha kuwa kabla ya maboresho hayo bandari hiyo ilikuwa kwa siku ikipokea wastani wa meli moja, lakini sasa meli nyingi zaidi zimekuwa zikitia nanga.
"Leo kuna meli zipo zinapakia mizigo, moja ni ya tani 9,000 na nyingine ni tani 30,000. Kesho zitakuja meli zingine tatu zitakazofanyakazi kwa wakati mmoja. Vitendea kazi vimeongezeka zaidi na vingine vitaletwa hapa kutoka Bandari ya Dar es Salaam ambako mwekezaji ameleta mitambo mingine," alisisitiza.
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imeibuka kidedea baada ya kufanikiwa kunyakuwa Ubingwa wa Jumla wa Mashindano ya SHIMMUTA kwa mwaka 2024 katika michuano iliyofanyika jijini Tanga.
Katika mashindano hayo ambayo yalifungwa rasmi na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo, yalishuhudia timu nne za TPA zikitawazwa mabingwa rasmi wa mashindano hayo.
Timu ya kwanza kutwaa ubingwa wa mashindano hayo, ni timu ya mpira wa kikapu ya TPA ambayo iliichabanga timu ya NSSF kwa jumla ya vikapu 57 - 45 katika mchezo wake wa fainali. Ubingwa huo ni wan ne mfululizo kwa kwa timu hiyo ya TPA.
Katika mchezo wa mpira wa pete “Netball” timu ya TPA ilitwaa ubingwa huo kwa kuifunga timu ya TMDA kwa magoli 53 – 43 katika mchezo wa fainali ya mashindano hayo. Huo ukiwa ni ushindi wanne mfululizo kwa timu hiyo ya TPA kutawazwa mabingwa wa mashindano hayo kwa mchezo huo.
Kwa upande wa mchezo wa kuvutana kwa Kamba, timu ya wanawake na wanaume zote za TPA, zilishinda michezo yao ya fainali, ambapo timu ya wanawake iliikung’uta timu TPDC, huku wanaume wakiigalagaza timu ya TBS kwa kuichapa katika mtanange uliozikutanisha timu hizo. Timu zote mbili za TPA zimetwaa ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo.
Na kwa upande wa mchezo wa riadha, timu ya TPA ilishinda katika mbio za mita 200 na kujinyakulia medali za dhahabu, huku katika mikimbio ya wazee ya mita 100, timu ya TPA iliibuka kidedea kwa kupata ushindi wa pili na kujinyakulia medali ya fedha.
Katika michezo ya jadi, timu ya TPA haikuondoka mikono mitupu kwani mwanamama Celine Simon alionyesha umahili wake kwa kuibika mshindi wa tatu katika mchezo huo wa.kusogeza kete yaani 'draft'.
Kufuatia ubingwa huo wa timu zake, TPA imeibuka mshindi wa jumla kwa mara ya pili mfululizo. Mara ya kwanza kuwa mshindi wa jumla ni mashindano ya mwaka 2023 yaliyofanyika mjini Dodoma. Katika mashindano yaliyofanyika mjini tanga mwaka 2024, jumla ya timu 96 kutoka taasisi za umma na binfasi zilishiriki.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, tarehe 26 Novemba 2024, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Ubelgiji, Wawekezaji, na Wafanyakazi wa Bandari ya Antwerp.
Ujumbe huo umeongozwa na Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Mhe. Peter Huyghebaert, pamoja na Balozi wa Tanzania katika Ufalme wa Ubelgiji na Jumuiya ya Ulaya, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga ambapo umetembelea Makao Makuu ya TPA katika Jengo la One Stop Centre, Jijini Dar es Salaam, na kukutana na Menejimenti ya TPA.
Katika mazungumzo yao, waligusia ushirikiano kati ya TPA na Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji katika maboresho ya huduma za kibandari, kulingana na mkataba wa ushirikiano uliopo kati ya TPA na Bandari hiyo. Mazungumzo hayo yalilenga kutoa ushauri elekezi wa kufanikisha mabadiliko chanya ya huduma za kibandari nchini pamoja na kuimarisha ushirikiano wa karibu na jumuiya hiyo.
Aidha, mazungumzo hayo yaligusia nia njema ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maboresho ya Bandari nchini ambapo Bw. Mbossa aliuelezea ujumbe huo kuhusu fursa zilizopo za uwekezaji katika Bandari zote nchini.
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"