Serikali ya Tanzania, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), imewekeza katika ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala, mradi wa kimkakati unaolenga kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya kuwa kitovu bora cha biashara kwa nchi jirani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Machi 16, 2025, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati wa ziara yake ya kikazi katika eneo la Bandari Kavu ya Kwala amesema bandari hiyo iliyopo Vigwaza, Kibaha, mkoani Pwani, ni suluhisho la muda mrefu kwa changamoto ya msongamano wa mizigo bandarini.
Ameeleza kuwa moja ya faida kubwa ya Bandari Kavu ya Kwala ni kupunguza muda wa kushughulikia mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuhifadhi makontena na shehena kubwa ya bidhaa Kwala, ufanisi wa bandari kuu utaongezeka, hivyo wateja kuhudumiwa kwa haraka zaidi.
“Hii itapunguza gharama za ucheleweshaji wa mizigo na kuimarisha mazingira bora zaidi ya biashara na uwekezaji nchini.”
Msigwa amesema bandari hiyo inatarajiwa kuhudumia makasha 823 kwa siku, yakiwemo yanayokwenda nchi jirani. Hii inamaanisha kuwa kwa mwaka itahudumia hadi makasha 300,395, sawa na asilimia 30 ya makasha yote yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam.
Aidha, amesema Serikali imewekeza katika miundombinu muhimu ili kuhakikisha ufanisi wa bandari hiyo, ikiwemo ujenzi wa reli ya mchepuko inayounganisha Kwala na Shirika la Reli Tanzania (TRC), barabara za zege, na mtandao wa umeme wa uhakika.
“Kupitia reli, mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam itaweza kusafirishwa moja kwa moja hadi Kwala, hatua itakayopunguza idadi ya malori barabarani, msongamano, ajali zisizo za lazima na kuokoa barabara zetu,” amesema Msigwa.
Mbali na hayo, Msigwa ameeleza kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu ndani ya eneo la mradi imekamilika kwa asilimia 80.
“Shughuli hizo zinahusisha na Mtandao wa barabara za zege zinazoweza kubeba malori ya mizigo, Jengo la kituo cha kupambana na moto, Jengo la utawala litakalohifadhi ofisi za mashirika ya serikali na watoa huduma za kitaalamu, Mfumo wa maji ya mvua, Mtandao wa umeme na maji safi, Hifadhi za viwanda zenye jumla ya mita za mraba 26,000 na Lango kuu na malazi ya wafanyakazi.”
Kadhalika Msigwa amesema bandari hiyo itakapokamilika, itakuwa na viwanda vikubwa na vya kati 200 pamoja na viwanda vidogo 300 vinavyohusika na Usindikaji wa vyakula, Utengenezaji wa vifaa, Viwanda vya dawa, Vifaa vya ujenzi, Usindikaji wa viatu na nguo, pamoja na Viwanda vya kemikali.
Kwa upande wa Kongani ya viwanda ya SINO-TAN, Msigwa amesema kuwa kongani hiyo itaongeza ajira kwa Watanzania ambapo inatarajiwa kutoa zaidi ya ajira za moja kwa moja 100,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 500,000. Mradi huu unajengwa kwa awamu tano.
Amesema hadi sasa, viwanda vitatu tayari vimeanza uzalishaji, vingine vitatu vipo katika hatua za mwisho za kufunga mitambo, na viwanda vinne vinatarajiwa kuanza ufungaji wa mitambo ifikapo mwisho wa Aprili 2025.
Mwisho

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepongezwa kwa kuweka mikakati ya kuwajengea uwezo Watumishi wanawake ili waweze kufanyakazi na kuleta matokeo chanya kwa Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ,Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha Bi.Sauda Msemo katika hafla ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani iliyoandaliwa na Wanawake watumishi wa TPA na kufanyika katika jengo la Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam Machi 15,2025.
Katika salamu zake za ukaribisho Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bw.Mbarikiwa Masinga kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA,amewataka Watumishi wanawake kufanyakazi kwa kushirikiana na kupendana bila kuwekeana chuki ili kufikia malengo makubwa ya Taasisi.
Awali akizungumza wakati akiwakaribisha wageni waalikwa katika hafla hiyo, Meneja Rasilimali Watu wa Bandari ya Dar es Salaam Bi.Mwajuma Mkonga amesema walizindua siku ya Wanawake Duniani kwa kupima afya za wafanyakazi na familia zao katika kituo cha afya kilichopo Bandarini na kutoa misaada ya vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 49 na kwamba TPA imekuwa ikifanya hivyo kwa miaka minne mfululizo.
Katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani Wanawake watumishi wa TPA walitoa misaada ya vifaa tiba katika hospitali za Wilaya ya Kigamboni vyenye thamani ya shilingi milioni 24 na hospitali ya Rufaa ya Temeke vyenye thamani ya shilingi milioni 25.
Pia katika kuadhimisha siku hiyo wameandaa Tuzo za Mabadiliko Chanya,mwanamke aliyebuni kitu kilicholeta mabadiliko na kuleta tija kwenye Taasisi.
Katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani,Watumishi wanawake wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wamebuni shindano la kugombea Tuzo ya Mabadiliko chanya, mchakato uliohitimishwa kwenye halfa iliyofanyika katika ukumbi wa jengo la Makao Makuu wa One Stop Centre jijini Dar es Salaam, Machi 15,2025.
Jaji wa Tuzo hizo Bi.Rosemary Ndesamburo alimtangaza Bi.Lucy Kalinga kuwa mshindi wa tuzo hizo zilizoanza kwa mara ya kwanza mwaka huu huku Bi. Farida Ismaili Hamisi alijinyakulia nafasi ya pili na Bi.Salma Kitwana akipata nafasi ya tatu.

Serikali ya Jamhuri ya Ireland imeeleza dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano wa kibiashara na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Bandari za Tanzania.
Kauli hiyo imetolewa Machi 14 2025 na Waziri wa Nchi, Mashauri ya Kigeni na Biashara wa nchi hiyo Mhe. Naele Richmond alipokutana na Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) jijini Dar es Salaam.
Katika salamu zake za ukaribisho Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Dkt. Baraka Mdima amesema, maboresho makubwa yaliyofanyika katika Bandari zote nchini yamechangia kuongeza ufanisi katika uhudumiaji wa shehena.

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imesema imeridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) katika Bandari ya Tanga hasa baada ya maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanywa na Serikali Bandarini hapo.
Kauli hiyo ya Kamati imetolewa tarehe 13 Machi,2025 na Mwenyekiti wake Mhe. Moshi Kakoso (Mb) baada ya kumaliza ziara yao ya kutembelea na kukagua miradi ya maboresho na miundombinu ya Sekta ya Uchukuzi katika Mkoa wa Tanga.
“Tunatoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais, Wizara ya Uchukuzi na TPA kwa maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga. Bandari sasa ufanisi unaonekana na mapato yameongezeka, hakika tumeridhishwa”. Amesema Mhe. Kakoso.
Mhe. Kakoso pia amesema kamati yake itaendelea kuisaidia TPA ili kutimiza maono ya Mhe. Rais na kufikia malengo yao na Serikali kwa ujumla.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile (Mb) ameishukuru Kamati kwa ziara yao iliyowawezesha kujionea kazi kubwa inayofanywa na Serikali Katika Sekta ya Uchukuzi. Aidha Mhe. Naibu Waziri Kihenzile ameihakikishia Kamati hiyo kuwa maoni, ushauri na maelekezo waliyoyatoa yatafanyiwa kazi ili kuhakikisha Mkoa wa Tanga unafunguka zaidi kiuchumi kupitia maboresho yanayoendelea kufanywa Miundombinu ya Uchukuzi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw.Plasduce Mbossa, amesema kukamilika kwa awamu mbili za maboresho ya Bandari ya Tanga kwa gharama ya shilingi Bilioni 429.1 kumekuwa chachu ya maendeleo na ufunguo kwa ushoroba wa Kaskazini.
“Manufaa mtambuka ya Bandari ya Tanga yatapelekea maeneo yanayozunguka bandari kufunguka kiuchumi hivyo ushirikiano na wadau wote ikiwemo Kamati yako Mheshimiwa Mwenyekiti ni muhimu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa”. Amesema Bw. Mbossa.
Pia Bw. Mbossa ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa TPA ili Mamlaka iweze kutekeleza mipango ya kuboresha miundombinu ya Bandari na kuwa chachu ya Maendeleo ya Uchumi wa Taifa. Aidha amesema TPA inathamini ushirikiano inaoupata kutoka Serikalini, Bunge na Wadau wote wa Sekta ya Bandari na itaendelea kusimamia bandari ya Tanga ili iendelee kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.

- WATUMISHI WA TPA WASHIRIKI KUTOA MISAADA YA VIFAA VYA TIBA KATIKA HOSPITALI ZA WILAYA YA KIGAMBONI NA TEMEKE
- TPA IMEKUTANA NA WAFANYABIASHARA KUTOKA NCHINI UHOLANZI
- BANDARI YA MTWARA YA HUDUMIA MELI YA SULPHR MV AFRICAN DIPPER
- BANDARI YA MTWARA YA ADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KIMKOA KATIKA VIWANJA VYA MASHUJAA
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"